SAKATA ya mauaji ya aliyekuwa
mwandishi wa habari wa kituo cha Chanel Ten mkoani Iringa marehemu Daudi
Mwangosi limeendelea kuchukua sura mpya mkoani Iringa baada ya askari
polisi anayetuhumiwa kuhusika na mauaji hayo kufichwa katika gari maalum
na askari wenzao.
Mtuhumiwa
wa mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa Chanel Ten mkoa wa
Iringa Daudi Mwangosi , askari mwenzao mwenye namba G2573 Pasificus
Cleophace Simoni (23) akiingia katika gari la polisi lenye namba za
usajili PT 1404 huku ulinzi ukiwa umeimarishwa kuzuia wanahabari
wasipige picha.
Tukio hilo lilitokea leo wakati mtuhumiwa huyo akifikishwa mahakamani
huku askari polisi hao muda wote wakionekana kuzunguka huku na kule
katika mahakama hiyo kama njia ya kuwathibiti wanahabari waliokuwepo
mahakamani hapo wasipate nafasi ya kumpiga picha mtuhumiwa huyo ambaye
ni askari mwenzao mwenye namba G2573 Pasificus Cleophace Simoni (23).
Hata hivyo kabla ya kuingia karandika
la mahabusu wengine, gari ya polisi aina ya Toyota lenye namba za
usajili PT 1404 likiwa na askari zaidi ya10 lilifika katika viwanja
hivyo vya mahakama na kuegeshwa pembeni likiwa ya mtuhumiwa huyo
aliyekuwa amefunikwa sura yake kwa kofia na kufichwa kabisa sura yake
kuonekana huku akiwa amekaa mbele kwa dereva akifichwa na askari
mwenzake pasipo kushuka.
Zikiwa zimebaki kama dakika 10
mahakama kuanza gari hilo lilisogea hadi mlango wa Mahakama na askari
waliokuwepo mahakamani hapo zaidi ya 20 kulizunguka gari hilo huku
wengine wakiwathibiti wanahabari akiwemo mwandishi wa habari hizi kama
njia ya kuzuia kupigwa picha kwa mtuhumiwa huyo na baada ya kuingia
ndani ya mahakama kabla ya hakimu kufika uthibiti ndani ya chumba cha
mahakama ulikuwa mkali zaidi dhidi ya wanahabari hasa wale wenye kamera.
Wakati huo huo Mahakama ya hakimu
mkazi wa wilaya ya Iringa imeahirisha kesi hiyo ya mauaji ya mwanahabari
Daudi Mwangosi ambae pia alikuwa ni mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa
habari mkoa wa Iringa (IPC). Mtuhumiwa huyo atafikishwa tena mahakamani
hapo Desemba 5 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.
Mwendesha mashitaka wa Jamhuri Adolf
Maganda aliieleza mnahakamani hiyo mbele ya hakimu Dyness Lyimo kuwa
mtuhumiwa huyo mnamo 02 Septemba mwaka huu katika kijiji cha Nyololo
Wilaya ya Mufindi Mkoa wa Iringa alimuua Daudi Mwangosi kwa makusudi
kinyume na kifungu cha sheria namba 148 kifungu kidogo 5A.i cha makosa
ya jinai.
Kwa mujibu wa kesi za jinai, sheria
kifungu 196 kanuni ya adhabu Cap. 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002,
kinakataza mtuhumiwa wa mauaji ya kukusudia kupewa dhamana.
No comments:
Post a Comment