Breaking

Post Top Ad

Your Ad Spot

Tuesday, October 16, 2012

PAKA ALIVYOTIKISA DARASA




MAKUBWA yamebainika kufuatia tukio la wanafunzi 12 wa Shule ya Msingi Vingunguti, Ilala, Dar es Salam kuanguka na kupoteza fahamu huku baadhi yao wakiweweseka baada ya kumuua paka aliyedondoka darasani shuleni hapo na kutikisa shule, Uwazi linakujuza yaliyo nyuma ya pazia.
Tukio hilo la kipekee na linalohusishwa na imani ya kishirikina, lilitokea Oktoba 12, 2012 wakati wanafunzi hao wakiendelea na masomo yao.
 
Mwanafunzi Happiness Mohamed aliyeshuhudia tukio hilo.
ETI KUNA UKWELI ULIOFICHIKA
Kwa mujibu wa vyanzo ndani ya shule hiyo, vyombo vya habari vingi vimeandika, lakini kuna ukweli uliofichika kuhusu paka huyo.
 Alisema tukio hilo lilishirikisha paka watatu ambao siku ya tukio saa nne asubuhi walizusha kilio cha kufa mtu katika dari la chumba cha darasa la sita mkondo C wakati wanafunzi  wakiwa darasani.
Inadaiwa wanafunzi hao walipatwa na hofu, ikabidi waache masomo kwani kitendo hicho hakijawahi kutokea shuleni hapo.
Wanafunzi hao wakiwa wanatafuta nini cha kufanya, walishangaa kuona paka mmoja amedondokea darasani huku akitoa harufu mbaya, ndipo baadhi yao walipochukua hatua ya kuokota mawe na fimbo na   kumpiga.
Taarifa zinaendelea kudai kwamba wakati paka huyo akipigwa, alikuwa akilia kama binadamu huku chumba cha darasa kikijaa moshi ambao haukujulikana ulikokuwa unatokea.
Baada ya paka huyo kukata roho tu, wanafunzi waliomuua walidondoka mmoja mmoja baada ya mwingine na kuanza kuweweseka huku baadhi yao wakipoteza fahamu, wale paka waliobaki kwenye dari wakazidi kulia kwa sauti ya juu, hali iliyosababisha kuwepo na vurugu ya hali ya juu darasani.
MWANAFUNZI ALIYESHUHUDIA
Mwanafunzi mmoja aliyeshuhudia tukio hilo, Happiness Mohamed wa darasa la nne mkondo C, alisema walimu waliwabeba waliozimia na kuwapeleka ofisini huku mwalimu  wa dini akiomba dua.
ALICHOSEMA MWALIMU
Naye mwalimu wa nidhamu wa shule hiyo, Innocent Mapunda alikiri kutokea kwa tukio hilo.
“Ni kweli  tukio hilo lilitokea hadi wazazi wakafika shuleni, kila mmoja akimtaka mwanaye aondoke naye, lakini wengine waliendelea na masomo kama kawaida hadi saa 8.
“Polisi nao walifika kutuhoji juu ya tukio hilo ambalo ni la kwanza kutokea hapa,” alisema mwalimu Mapunda.
HILI NALO VIPI?
Mzee mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja na Issa, mkazi wa Vingunguti, akizungumza na gazeti hili Ijumaa iliyopita alisimulia mazito.
“Wale wanafunzi kumi na wawili walikuwa wafe wao, salama yao ilikuwa ni vile walivyomuua paka. Huyu paka nyuma yake kuna mtu, maana hata baada ya kufa, alipokwenda kutupwa, baadaye hakukutwa tena eneo lile.
“Cha ajabu ambacho viongozi wetu wanakifumbia macho ni kwamba, siku ile paka anauawa na wanafunzi, usiku wake kuna mzee alifariki dunia. “Huyu mzee watu wengi walikuwa wakimtuhumu kwa ushirikina, sasa huoni kama kuna kitu nyuma ya kifo cha paka huyo?
 
Paka anayefanana na yule aliyedondoka darasani na kuuawa.
“Mwaka jana, kuna mkazi mmoja aliyekuwa anamiliki duka alipatwa na tukio la ajabu. Paka mwenye rangi ya kaki, alifika kwenye biashara yake, yule bwana akaokota jiwe na kumpiga, akakimbia lakini usiku wake yule bwana akafa, unaona mambo hayo?
“Sasa wale wanafunzi kama wangempiga yule paka halafu akafanikiwa kukimbia bila kufa, wangekufa wao, maana yule paka alikuwa muuaji na alikwenda pale ili kuua,” alisema mzee huyo mwenye umri wa miaka 73.
Naye mzazi wa mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo aliyezungumza kwa sharti la jina lake kutoandikwa gazetini, alisema mara baada ya kusikia kuwa kuna paka shuleni na watoto wanaanguka, alikwenda haraka kumchukua mwanaye.
“Haya ni mambo ya kishirikina, haiwezekani paka asababishe moshi darasani, niliamua kwenda kumchukua mtoto wangu kwa hofu kuwa wachawi wanaweza kusababisha vifo vya watoto wetu, yupo mtu alikufa kwa sababu ya mambo hayahaya ya paka mwaka jana,” alisema.
KAMANDA WA POLISI AONGEA
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi, Ilala, Marietta Komba alipoulizwa  juu ya tukio hilo alikiri  kutokea lakini hakutaka kwenda mbele zaidi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages