kili stars |
Mabao mawili yaliyowekwa kimiani na
mkongwe Robert Ssentongo pamoja na jingine lililozamishwa kimiani na
Emanuel Okwi, dhidi ya Kilimanjaro Stars, yameiwezesha timu ya soka ya
taifa ya Uganda kutinga hatua ya fainali ya michuano ya mwaka huu ya
Nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, na kuinyima timu ya Taifa ya
Tanzania Baramaarufu kama CECAFA Challange Cup 2012.
Katika mechi hiyo ambayo imemalizika
hivi punde, Kilimanjaro Stars, ambayo ni timu ya Taifa ya Tanzania Bara,
ilikosa kabisa mbinu zilizowafanya kuonekana kama moja ya timu ambazo
zingeweza kutwaa michuano hiyo, kwani ilishindwa kabisa kuonyesha
kandanda la kiwango cha juu kama walivyofanya katika mechi za awali
kuelekea nusu fainali hiyo.
Uzembe wa mabeki wa Kilimanjaro Stars,
kufa kwa sehemu ya kiungo sanjari na staili ya kucheza mipira mirefu,
vilikuwa sababu kubwa za Kilimanjaro Stars kupoteza mechi hiyo, ambapo
uzembe wa mabeki ndio uliosababisha Emanuel Okwi, kufunga bao la kwanza
kunako dakika ya 10 ya mchezo, baada ya kuwatoka mabeki wa Kili Stars na
kuachia shuti maridadi lililomshinda mlinda Mlango Juma Kaseja.
Kuingia kwa bao hilo ambalo lilidumu
hadi muda wa mapumziko, pamoja na muda wa dakika 15 za mapumziko,
havikutumika sahihi na wachezaji na kocha wa Kili Stars, ili kupanga
mkakati mpya wa kuhimili vishindo vya Uganda, na walirejea uwanjani
kipindi cha pili wakiwa kikosi kisichostahili kupata ushindi katika
mechi hiyo.
Ni kukosa huko malengo ambako kulimpa
nafasi Ssentongo nafasi ya kuzamisha mabao yake mawili kunako dakika za
51 na 72, mabao ambayo yalipelekea mchezo huo kumalizika kwa Uganda 3-0
Kilimanjaro Stars.
Kwa matokeo hayo, Uganda wameendeleza
rekodi ya kutofungwa bao hadi wanapofikia hatua ya fainali, na
watapambana na Kenya katika mechi ya Fainali, huku Kili Stars
wakitarajiwa kuumana na Zanzibar Heroes, katika mechi ya kuwania mshindi
wa tatu. Zanzibar waliondoshwa na Kenya kwenye nusu fainali, kwa
matuta, katika mechi ambayo ilikuwa imechezwa awali.
No comments:
Post a Comment